mobile header
11 March 2019 Utafutaji wako una athari gani?

Je, wajua kuwa unapotiririsha filamu mtandaoni, au unapotafuta jibu la swali fulani, unaathiri mazingira?

Kila SMS au barua pepe unayotuma; kila picha unayopakia…

Story

Je, wajua kuwa unapotiririsha filamu mtandaoni, au unapotafuta jibu la swali fulani, unaathiri mazingira?

Kila SMS au barua pepe unayotuma; kila picha unayopakia kwenye wingu au faili ya dijitali unayotuma, inaathiri mazingira.

Mara nyingi huwa tunachukulia intaneti—inayotusaidia kutekeleza mengi muhimu—kuwa wingu lisilo na kaboni linalohamisha data kupitia hewa. Hata hivyo, intaneti inategemea rasilimali nyingi kwenye mazingira. Kebo zilizo chini ya ardhi zinatumika kusambaza umeme kwa vituo vya data, na mashine mbalimbali zinazoendesha utafutaji wetu mtandaoni mara nyingi hutegemea nishati za kisukuku.

Kwa mujibu wa shirika la Greenpeace, sekta ya habari na teknololojia kote ulimwenguni hutumia takriban asilimia saba ya kiwango cha umeme kinachotumika kote ulimwenguni. Mwaka wa 2015, utiririshaji video ulichangia karibu asilimia 60 ya utumiaji wa intaneti kote ulimwenguni na kiwango hiki kinatarajiwa kuongeza hadi asilimia 80 kufikia mwaka wa 2020.

“Intaneti ni mtambo usioonekana,” alisema Mark Radka, mkuu wa kitengo cha kawi na hali ya hewa cha idara ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa. “Hatuoni mfumo mzima unaoendesha shughuli zetu mtandaoni, na mara nyingi, hatufahamu jinsi shughuli hizi zinavyotekelezwa. Hii ina maana kuwa hatutafakari jinsi zinavyoathiri mazingira.”

image
INTANETI IMEKUZA UTUMIAJI NISHATI KATIKA SEHEMU NNE KUU AMBAZO NI: VITUO VYA DATA, MITANDAO YA MAWASILIANO, VIFAA VYA WATUMIAJI KAMA VILE SIMU ZA MKONONI NA UTENGENEZAJI.  

Imekua zaidi, lakini je, ni bora?

Intaneti imekuza utumiaji nishati katika sehemu nne kuu ambazo ni: vituo vya data, mitandao ya mawasiliano, vifaa vya watumiaji kama vile simu za mkononi na utengenezaji—uundaji wa vifaa hivi.

Uvumbuzi unaendelea ili kuboresha vituo vya data na kubuni mbinu mpya za kuokoa nishati tofauti na mbinu za kawaida za uingizaji hewa. Google kwa mfano, imeripoti kuwa vituo vyake 14—vinavyoendesha Gmail, YouTube na Tafuta na Google kote katika kontinenti nne—huokoa asilimia 50 ya nishati ikilinganishwa na kiwango kinachotumiwa na vituo vya kawaida.

Kwa mujibu wa Google, ikilinganishwa na miaka tano iliyopita, utendakazi wa vituo hivi umeongezeka mara saba kwa kutumia kiwango kile kile cha umeme. Alibaba, kwa upande wake, hutumia maji ya ziwa asili kupoza seva katika kituo kimoja na mnara wa kuzungusha hewa katika kituo kingine.

Huenda intaneti ndicho kitu kikubwa zaidi kuundwa na binadamu—na inaendelea kukua zaidi. Baadhi ya watafiti wamebashiri kuwa utumiaji intaneti utaongezeka mara tatu kufikia mwaka wa 2020: tunahitaji kubuni mbinu mpya  za kudhibiti matumizi yetu wa mtandao.   

“Kufahamu tu kuwa kuvinjari intaneti kunaathiri mazingira ni hatua muhimu ya mwanzo,” alisema Radka. “Kampuni zinaposhinikizwa na wateja wake, hupea kipaumbele suala la uwajibikaji kimazingira na usambazaji unazingatia maadili jamii na mazingira.”

Kutokana na suala la kubadilika kwa hali ya hewa ulimwenguni, wateja wanazidi kutafuta nishati mbadala hivyo kupunguza gharama za nishati.

Kampuni shindani zinazingatia suala la uhifadhi wa mazingira. Kampuni kubwa za intaneti kama vile Apple, Facebook na Google zinatumia nishati mbadala kwa asilimia 100, hivyo kupunguza taka na viwango vya nishati zinavyotumia.

image
WATEJA WANAZIDI KUTAFUTA NISHATI MBADALA, HIVYO KUPUNGUZA GHARAMA.

Kutumia data kuhifadhi mazingira

Kwa kiwango kikubwa, maboresho haya yanahusu hasa uzalishaji bora na mahiri zaidi.

Erick Litswa, meneja wa Mfumo wa Habari wa Kuripoti kuhusu Hali ya Mazingira wa Idara ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa, anasema kuwa uchambuzi wa kina unahitajika katika suala la uboreshaji.

Data—uchanganuzi wake na kuweza kuifasiri ni mchakato unaozidi kuwa muhimu zaidi. Kushiriki data muhimu ni wajibu wa kila mmoja wetu, na hivi ndivyo kampuni kubwa za intaneti zinavyoweza kutoa huduma muhimu kwa watu wote ulimwenguni, alisema Litswa.  

“Miaka ishirini iliyopita, ulipokuwa na swali huenda ungewauliza watu 10 kijijini. Leo, algoriti na kipengele cha mashine kujifunza vinatumika kutafuta majibu sahihi kote ulimwenguni kwa sekunde chache.

“Hali hii imeboresha utafutaji data. Kushiriki data hii kunaweza kuleta manufaa mengi kwa mazingira. Kwa mfano, picha za sateliti zinaweza kutusaidia kufuatilia ukataji miti, au ambako maji yanavuja au kupotea, hivyo kutuwezesha kumakinika jinsi tunavyotumia maji.”  

Baadhi ya mashirika yanatekeleza zaidi. Wanaoendesha mtambo wa kutafuta wa Ecosia wanasema kuwa wanapanda miti katika sehemu mahususi ili kufidia viwango vya kaboni vinavyotumika kwa utafutaji. Hata hivyo, mipango ya kufidia kaboni haisawazishi kikamilifu viwango vinavyotumika.

Kwa hivyo, tunapaswa kutumia nishati kidogo. Japo hali ya sasa siyo ya kuridhisha, tunaweza kujizatiti ili kupunguza utumiaji wa intaneti. Kupunguza muda tunaotumia kwenye mtandao ni mwafaka utakaofaa sayari yetu na vilevile utakaokufaa.

Katika Baraza la Mazingira ya Umoja wa Mataifa, Idara ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa inawahimiza watu Kupanua Mawazo na Kuishi kwa Uwajibikaji. Jiunge na mjadala kwenye mitandao ya kijamii kwa kutumia #SolveDifferent kushiriki hadithi zako na kuona mambo ambayo watu wengine wanafanya ili kuhakikisha mustakabali endelevu wa sayari yetu.

Recent Stories
Press release

Zaidi ya watu 4,700 wamekusanyika ili kubuni sera mpya, teknolojia na ufumbuzi bunifu wa kutimiza matumizi na uzalishaji endelevu. Matokeo kutoka…

Press release

Takriban watu 2,000  – wakiwemo watu wenye vyeo vya juu kutoka IBM, Google na Barclays – wanahudhuria Kikao cha Pili cha Dunia cha Kongamano…